AINA YA WATU KILA MTU ANAOWAHITAJI ILI KUFIKA MBALI KIMAFANIKIO:


Kuna watu katika maisha yako unawahitaji kama kweli unataka kufanikiwa.Hii inamaanisha unahitaji kuwa makini na watu ambao unahusiana nao katika maisha yako ili watumike kama njia ya kukusogeza hatua kubwa ya mbele zaidi na sio kukurudisha nyuma ama kukuchelewesha kufika ambako unakwenda.Leo ningependa tuangalie kwa ufupi aina tatu za watu ambao lazima uwe nao katika maisha yako ili wakusaidie kufanikiwa kwa haraka:
1. Watu wa kukuwajibisha (Accountability Partners).

Hawa ni aina ya watu ambao kila wakati unapowafikiria wanakuwa wanakupa hamasa ya kutimiza na kutekeleza kile ambacho ulikusudia na ulisema utakifanya.Mara nyingi watu hawa huwa hawaji “automatic” bali huja kwa wewe kudhamiria kuwa nao katika maisha yako.
Hawa ni muhimu sana hasa pale unapopanga mipango yako ya maisha na malengo yako ya mafanikio.Hawa ndio wale ambao wanaweza kukupigia simu na wakakuuliza “ile biashara uliyosema utaanza kuifanya mwezi huu mbona bado haujaanza”?.Watu wa namna hii kila ukiwakumbuka hata kama umechoka unajikuta unajilazimisha kufanya-Huwa wanakuwa kama vile wanavyokuwa mabosi kazini-Ukipewa ripooti ya muhimu hata kama siku hiyo ni mechi ya fainali kombe la dunia na wewe ni mshabiki mkubwa wa mpira wa miguu,utajikuta unatafuta mbinu yoyote hadi unamaliza ripoti yako.
Huyu ni mtu ambaye ukisema kuwa umeacha kutumia pesa zako vibaya,akikuona unaendelea kutumia vibaya atakukumbusha ahadi yako,—Na kwa sababu ni mtu unamuheshimu utajikuta kila saa haupendi kumuangusha.Kama hauna mtu wa kukuuliza tangu January kuhusu mipango yako na jinsi ya kuifanikisha basi ujue bado hauna mtu wa namna hii ninayemzungumzia hapa.
Mara nyingi mtu wa namna hii anatakiwa awe ambaye hauko tayari kumuangusha kwa kutofanya ulichosema kuwa utafanya.Mtu ambaye hana mtu wa kuwajibisha ni sawa na kuwa na magari baranarani bila kuwa na askari wa usalama barabarani.Kama katika maisha yako hauna mtu wa namna hii basi kwako itakuwa ni rahisi sana kupoteza mwelekeo.
2. Mlezi wa Ndoto zako(Mentor)

Huyu ni mtu muhimu sana katika maisha yako.Watu wengi sana huchanganya “role model” na “Mentor”.Role model ni mtu ambaye unatamani sana kuwa kama yeye kutokana na kile alichofanya na wewe unatamani pia kukifanya na ufikie viwango ambavyo yeye amevifikia.Lakini mentor ni mtu ambaye anakusaidia kulea ndoto zako kwa kukupa mwongozo,ushauri na kukuonya na kukurudidha kwenye mstari.Watu wengi sana huwa hawapendi kuwa na mtu wa namna hii kwenye maisha yao kwani hufikiri kwa kufanya hivyo basi watapoteza uhuru wao,lakini ukweli ni kuwa kama unataka kufika mbai basi lazima umtafute mtu wa namna hii.
Katika uhalisia unaweza kuwa na mentors zaidi ya mmoja kwenye maeneo mbalimbali kama vile-Kiroho,kiuchumi,kitaaluma n.k.Jambo kubwa sana kuhusu mentor wako ni kuwa anakuwa na hekima na maarifa ya kukusaidia hasa katika kukupa mwongozo wa namna ya kufikia kule unakotaka kwenda.Kwa kawaida lazima awe mtu ambaye unamwamini na unaweza kujifunua wazi kwake kuhusu maisha yako.
3. Watu mnaoelelekea njia moja (Reference Group)

Katika kila ambacho unatamani kufanya katika maisha yako,ni lazima kuna watu ambao nao pia wanatamani kuelekea njia hiyiyo.Lakini utakachogundua ni kuwa kuna wengi ambao watakuwa wako mbele yako tayari na wengi ambao wako nyuma yako pia.Aina hii ya watu ni muhimu ili kubadilishana uzoefu na kutiana moyo ili wote muweze kufika kule ambako mmekusudia kwenda.
Aina hii ya watu ianweza ikwa sio rahisi kuonana nao kila siku lakini ni muhimu kukutana nao baada ya muda fulani ili muweze kwa pamoja kujifunza kila mmoja kutoka kwa mwingine.Jaribu kuchunguza kwa watu ambao wanakuzunguka na tafuta watu angalau watano ambao utawafanya kuwa reference group yako kwa mwaka 2017.Jaribu kupanga mikakati na wao kisha mkubaliane muwe mnakutana kila baada ya muda gani kuanzia january.
Pata Kitabu cha TIMIZA MALENGO YAKO ili ujifunze zaidi namna ya kufanikisha mipango yako ili kufikia kilele cha mafanikio katika maisha yako.


See You At The Top.
Oldest